Love & Relationships

Nyar Afrika: Mbona inatubidi kuzungumza kuhusu ubakaji wa kisagaji

Posted By

On Jul 30, 2019

For the english click here.

Kiwango kipi kinazidi? Jambo lipi linatokea anapokataa? 

Nyote wawili mumejiandaa kwa siku hii; jumbe za kutongozana, ishara hapa na pale, ghafla muda unawadia, mnatimia kupeana busu naye anasema kuwa hayuko tayari. Haimsisimui. Unafanyaje? Utachukua hatua gani? Utashughulikia tukio hili vipi?

Haya ni baina ya maswali mengi wanayowaza wanawake wanaofanya ngono na wanawake wenza punde wenzao wanapokataa kutongozwa dakika ya mwisho.

Japokuwa kunao watu watakaoelewa na kuheshimu msimamo wa mwenzio, hata kuwapa nafasi na heshima wanayoitaka, wengine huendelea kufanya ngono nao bila idhini yao.  

Ngoja, ngono bila idhini ya mtu? Je, tendo hilo sio ubakaji? Je, wanawake huwabaka wanawake wengine? Jambo hilo linawezekana? Huwa linatendeka? 

Ndio, ni ubakaji, hutendeka, linawezekana mno na wanawake huwabaka wanawake wengine. 

Ubakaji wa mwanamke mwenza; shambulizi kwa usisimuaji wa lazima wa sehemu nyeti za mwanamke kwa uhalifu wa msagaji kwa kutumia mitandao, ngono ya kinywa, kichezeo cha ukanda, vifaa vingine au usuguaji uke kwa uke.

mara nyingi tunapozungumza kuhusu ubakaji, tunauhusisha na mhalifu mwanaume tukisahau kuwa wanawake pia huweza kuwa wahalifu. Jambo hili linaonekana katika tovuti zinazohudumia kesi za ubakaji kwa matumizi ya viwakilishi vya kiume na kusababisha kizuizi. hili linawapa waathirika ono kwamba ubakaji wa kisagaji haiwezekani na kuwa ni tendo linalowezekana tu baina ya jinsia tofauti na kuwalazimu kulinyamazia bila kulishtaki, kulizungumzia wala kusaka usaidizi wa kitaalam. 

Ubakaji wa kisagaji  unaathiri wengi wetu kwenye jamii ya wasenge ijapokuwa hatuujadili kamwe kwa hofu ya fedheha, kutoeleweka au kudhihakiwa.”

Jo Harvey Barringer,Mkurugenzi wa ‘Broken Rainbow’, mhisani wa pekee dhidi ya unyanyasaji wa kinyumbani nchini Uingereza, amekiri kuwa wasenge kujitambulisha ni swala zito. “Utamwabia vipi” asema “mtu yeyote ya kuwa umebakwa na kuishi katika hofu iwapo hakuna anayejua wewe ni msenge?”

Je, ni madhara yepi yanawafikia waathirika wa ubakaji wa kisagaji duniani?

Kulingana na Shirika la Upelelezi la Marekani na Idara ya Haki ya Marekani, asilimia sabini na tano ya waathirika wa ubakaji wanahitaji matibabu baada ya uhalifu huo. Idadi nusu ya waathirika huuguza majeruhi yasiyosababishwa na tendo la ubakaji. Katika asilimia thalathini ya ubakaji, silaha hutumiwa dhidi ya mwathirika.  

Idara ya Haki na Shirika la Upelelezi la Marekani wanataja ubakaji kuwa na idadi zaidi ya hatia zote (mwanamke hubakwa kila dakika mbili Marekani.) Vilevile, zaidi ya idadi nusu ya visa vya ubakaji hutendwa na mtu anayefahamiwa na mwathirika. Huenda ikawa mpenzi, rafiki au hata msiri mwaminiwa. Sana sana, asilimia ishirini na tano ya idadi ya ubakaji hutendwa na mwenzi mwaminiwa wa mwathirika.  

Shirika la Upelelezi la Marekani linakisia ya kwamba asilimia thalathini na saba tu ya visa vya ubakaji hushtakiwa kwa polisi. Sababu kuu inayotolewa na waathiriwa kwa kutoshtaki visa hivi ni mhalifu kulipiza. 

Hapa Kenya, ubakaji wa kisagaji kamwe haishtakiwi. Sababu ikiwa hofu ya kutakikana kuelezea matukio kwa kina kwani ukihitaji usaidizi, lazima utoe maarifa kuhusu mhalifu na mara nyingine, aina ya uhusiano baina yako na mhalifu.

Kushtaki kisa cha ubakaji katika jamii ya kisagaji inakubidi kujivumbua kuwa msagaji. Hili linawaweka waathiriwa wengi katika hatari ya kudhihakiwa na kutengwa. Inamaanisha kuhimili maswali ya wenye mamlaka kwa mfano “Ooh! Kwa hivyo wewe hulala na mwanamke?”  

Ni vigumu zaidi kupata usaidizi kwani ni hatia kuwa na uhusiano wa kingono na mwanamke mwengine. Mja anakumbwa na hofu ya kujivumbua, shauku au kutojali na uhasama wa polisi, kusita kuwasaliti wenzao katika jamii ya wasagaji, kufedheheshwa na jamii na mwono kuwa ubakaji wa kisagaji hauchukuliwi kwa uzito unaochukuliwa ubakaji uliotendwa na mwanaume. Haya ni baina ya sababu nyingi zinazowasababisha manusura kusita kushtaki ubakaji wa kisagaji.    

Ukosefu wa mazungumzo kuhusu uhasama wa kijinsia katika jamii ya LGBT unahuzunisha. Unyamavu huu unatokana na aibu, aibu inayohusishwa na kubakwa, kuchapwa au uhasama wa kijumla. Jamii ya wasagaji inapaswa kuwa yenye umoja kwa kuwa tuko wachache, daima tunalengwa kwa sababu ya mapendezi yetu ya kingono na ndio maana ni muhimu kwetu kujihisi kuwa salama miongoni mwa wenzetu.

Je, tunatatuaje ubakaji wa kisagaji na kwenye hali nyingine, ubakaji baina ya wanawake wenye mapendezi ya jinsia mbili ambao hujihusisha na wasagaji? 

Tuwape manusura nafasi yenye usalama. Nafasi itakayowawezesha kutafuta usaidizi bila kuhukumiwa jinsi walivyo. Tuvunje unyamavu. Tuwe na majidiliano kuhusu uhasama katika jamii ya wasagaji na kutafuta suluhisho za kuutatua.

Tumpe sikio yeyote anayehitaji usaidizi wetu. Tuwasaidie wanaonyanyaswa. Tuwe waangalifu kwa niaba ya wenzetu. Tuwaenzi ndugu zetu.  

Tuungane mikono kusitisha ubakaji wa kisagaji.

Nyar Afrika inatafsiriwa kumaanisha binti wa Afrika. Yeye ni mwandishi msagaji mwenye miaka ishirini na moja kutoka nchi ya Kenya 

Facebook: NYAR Afrika
Twitter: @NyarAfrika
Instagram: @beryl_opiyo

Kifungu hiki kilichapishwa mwanzo katika The Rustin Times.

This piece forms part of  the #QueeringTheCloak series which is part of a larger project exploring sexual, emotional and physical violence in queer women spaces on the continent.  The project seeks to essentially ‘pull back the cloak’ on shame and silence around this violence.